IQNA

Magaidi wakufurishaji wa Boko Haram waua askari 10 Niger

22:00 - July 02, 2018
Habari ID: 3471580
TEHRAN (IQNA)-Magaidi wakufurishaji wa Boko Haram wameua askari kumi wa Niger katika hujuma kusini mashariki mwa nchi, karibu na mpaka na Nigeria.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger, Abdoul-Aziz Toure amesema, shambulizi hilo la Jumapili lilifanyika katika kijiji cha Bla Brin, yapata kilomita 40 kutoka mji wa N'Guigmi, karibu na eneo la Ziwa Chad, ambapo wapiganaji wa Boko Haram walishambulia ngome za askari hao.

Amesema askari kumi wamethibitisha kupoteza maisha, huku wengine wanne wakitoweka, isijulikane iwapo walitekwa nyara na wanachama wa genge hilo la ukufurishaji au la.

Juzi Jumamosi, magaidi wa kundi la Boko Haram walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani ya nchi,  katika hujuma waliyotekeleza katika eneo la mpaka wa Nigeria na Cameroon ambapo watu wasiopungua wanne waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Mapema mwezi jana wa Juni, watu tisa waliuawa katika mashambulio kadhaa ya mabomu huko kusini mashariki mwa Niger karibu na mpaka wa nchi hiyo na Nigeria, hujuma zinazoaminika kufanywa na Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi hilo lenye itikadi za Kiwahhabi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo. Serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria imeshindwa kuwaangamiza magaidi hao huku baadhi ya majenerali jeshini wakituhumiwa kuwa wanafaidika na kuendelea vitendo vya kigaidi nchini humo.

3466201

captcha