IQNA

Msichana mwenye ulemavu wa macho na saratani ahifadhi Qur'ani kikamilifu

16:54 - July 14, 2018
Habari ID: 3471593
TEHRAN (IQNA)- Msichana Mmisri mwenye ulemavu wa macho na ambaye pia aliugua saratani amehifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu.

Hanine Ashraf Abulaynein Muhammad ni binti mwenye umri wa miaka 9 ambaye mfano wa wazi wa ule usemi usemao ulemavu sio kutoweza kwani alianza kuhifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka mitatu na sasa amefanikiwa kuhifadhi kikamilifu kitabu hicho kitakatifu.

Hanine aliugua saratani akiwa na umri mdogo wa miezi tisa tu na baada ya miezi miwili akapoteza uwezo wake wa kuona kutokana na ugonjwa huo. Lakini hilo halikuwa kizingiti katika azma yake ya kujifunza Qur'ani Tukufu. Aliwanikiwa kuhifadhi Qur'ani kikamilifu akiwa na umri wa miaka saba na hivi sasa yuko darasa la nne katika Shule ya Msingi ya Al Azhar katika jimbo la El Sharqia  nchini Misri. Hadi sasa Hanine amefanikiwa kushinda mashindano ya Qur'ani Tukufu kieneo na kitaifa.Msichana mwenye ulemavu wa macho na saratani ahifadhi Qur'ani kikamilifu

Mama yake Hanine, Itimad Fathi anasema binti yake alianza matibabu yake ya saratani akiwa na umri wa miezi tisa na alifanyiwa upasuaji mara kadhaa. Anasema madaktari walimfahamishwa kuwa kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu hali yake iliboreka na kwamba jambo hilo lilikuwa ni sawa na muujiza.

Naye Ashraf Abou El Ainein, baba yake Hanine anasema: "Hunain alianza kuhifadhi Qur'ani akiwa na umri wa miaka mitatu na wakati huo waalimu wengi katika madrassah za Qur'ani walikataa kumpokea kutokana na umri wake mdogo. Kwa msingi huo mama yake ndie aliyemfunza Juzuu ya kwanza.  Alipofika umri wa miaka mitatu na nusu alienda katika madrasah mtaani kwetu. Hatimaye alipofika umri wa miaka mitano aliweza kuhifadhi robo moja ya Qur'ani Tukufu. Wakati huo pia alishiriki katika mashindano kadhaa ya Qur'ani na kushika nafasi ya kwanza."Msichana mwenye ulemavu wa macho na saratani ahifadhi Qur'ani kikamilifu

Abou El Ainein anaongeza kuwa: "Hatimaye, Hanine aliweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu akiwa na umri wa miaka saba. Ameshiriki aktika mashindano 15 ya Qur'ani katika mji wa El Qurein na pia katika mkoa wa El Sharqia  na halikadhalia kitaifa. Ameweza kufanya vizuri katika mashindano hayo yote na kwa miaka mitatu mfululizo amekuwa akishika nafasi ya kwanza katika mashindano ya kituo cha Al Azhar."

3729161

captcha