IQNA

Chakula Halali kufika katika anga za juu

23:00 - July 07, 2019
Habari ID: 3472033
TEHRAN (IQNA) - Shirika moja la anga za mbali la nchini Russia ambalo hutayarisha chakula cha wanaanga (astronauts) kimesema kitaanza kutayarisha chakula halali maalumu kwa ajili ya Waislamu.

Kwa mujibu wa taarifa shirika la Space Food Laboratory limesema litatayarisha chakula halali ambacho kinatazamiwa kutumiwa na mwanaanga wa kwanza kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambaye ataelekea katika Kituo cha Anga za Juu cha Kimataifa (ISS) baadaye mwaka huu.
Shirika hilo la Russia limesema litampa mwanaanga huyo wa UAE chakula halali cha makopo ambacho kitajumuisha chakula cha utamaduni wa Kiarabu kikiwemo balaleet, sluna na madrouba.
Mwanaanga wa UAE, Hazza Mansouri anaendelea na mazoezi ya kuelekea anga za juu nchini Moscow. Mansouri anatazamiwa kuelekea katika Kituo cha Anga za Juu cha Kimataifa mwezi Septemba akiwa na mwanaanga wa Russia Oleg Skripochka na mwingine wa Marekni Jessica Meir wakitumia chombo cha kusafiria anga za mbali cha Russia aina ya Soyuz MS-15.
Mwanaanga huyo wa UAE anatazamiwa kuwa katika anga za mbali kwa muda wa siku nane ambapo atatekeleza majukumu kadhaa kama vile kuchunguza sayari ya dunia, upigaji picha na kuchunguza maisha ya kawaida ya wanaanga katika ISS.

3825013

captcha