IQNA

Spika wa Bunge la Iran ataka hatua zichukuliwe kusitisha uhasama wa Israel

14:05 - July 02, 2020
Habari ID: 3472922
TEHRAN (IQNA) - Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua athirifu za kukomesha jinai za utawala haramu wa Israel, hususan mpango wa utawala huo ghasibu wa kupora ardhi zaidi za Wapalestina.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran ametoa mwito huo katika jumbe tofauti alizowaandikia wakuu wa taasisi za kimataifa, wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel unajiandaa kutwaa ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika ujumbe huo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres na Rais wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU), Gabriela Cuevas Barron, Qalibaf ameashiria msimamo thabiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutaka kukomeshwa ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina, na hatua za kichochezi na haramu za utawala pandikizi wa Israel, zinazohujumu amani na usalama wa dunia.

Aidha Spika wa Bunge la Iran amewatumia ujumbe kama huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Mohammed Qureshi Nias, Katibu Mkuu wa OIC, Yusuf bin Ahmad al-Uthaimeen na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mabunge ya Asia, Mohammad Reza Majidi.

Mohammad Baqer Qalibaf amewataka wakuu hao wa taasisi za kimataifa kuchukua hatua zinazoendana na sheria za msingi za haki za binadamu zilizobainishwa kwenye Hati ya Umoja wa Mataifa, katika kukabiliana na sera haribifu za kujitanua za utawala ghasibu wa Israel.

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, hatua hizo batili zinazochukuliwa na utawala katili wa Israel zinakanyaga wazi wazi sheria za kimataifa na nyaraka za Umoja wa Mataifa hususan Azimio Nambari 2234 la Baraza la Usalama la umoja huo. Amesema chokochoko hizo mpya za Tel Aviv zinapaswa kutazamwa kama uvamizi mpya dhidi ya Wapalestina na turathi zao za kihistoria.

3908070

captcha