IQNA

Rais Rouhani: Ni jukumu la kidini kutangaza iwapo umeambukizwa corona

20:00 - July 04, 2020
Habari ID: 3472929
TEHRAN (IQNA) – Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ni jukumu la kidini kwa kila mtu kutangaza iwapo ameambukizwa kirusi cha corona (COVID-19) ili kuzuia maambukizi kwa wengine.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo Jumamosi mjini Tehran katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kupambana na ugonjwa wa corona na kuongeza kuwa ni jukumu la kidini kwa aliyeambukizwa corona kuwajulisha wengine, hasa jamaa katika familia na wafanyakazi wenzake.

Rais wa Iran amesema mtu anaweza kuambukizwa COVID-19 kwa njia mbali mbali na iwapo atabaini ana ugonjwa huo basi awafahamishe wengine na ajiweke karantini kwa muda wa wiki mbili ili kuokoa maisha ya wengine.

Halikadhalika Rais Rouhani amezungumzia tadibiri na mipango imara humu nchini katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 na kusema kuwa, Iran imefanya kazi kubwa katika kudhamini dawa na vifaa vya tiba na matibabu.

Huku akilinganisha hali ya kiuchumi ya dunia kabla na baada ya corona na hatua za tiba na matibabu zilizochukuliwa na nchi mbalimbali duniani amesema, Iran imeweza kujitegemea na kusimama imara katika kujidhaminia dawa na vifaa vya matibabu katika kipindi hiki kigumu cha ugaidi wa kiuchumi na kimatibabu wa Marekani dhidi yake na imefanikiwa kufanya kazi kubwa ya kujivunia katika jihadi hiyo.

Vile vile amesema, hatua za sasa hivi zinazochukuliwa na serikali yake ni kupiga marufuku kutolewa huduma zozote katika taasisi za Serikali iwapo wanaotaka huduma hizo hawatochunga protokali za afya na iwapo hawatokuwa wamevaa barakoa. Amesema ili kuweza kuvuka kwenye kipindi hiki kigumu inabidi wanaotoa na wanaopatiwa huduma wote wachunge misingi ya afya ikiwa ni pamoja na wote kuvaa barakoa.

Aidha Rais Rouhani amewapongeza na kuwashukuru pia wanasayansi wa Iran wanaofanya jihadi katika uzalishaji wa dawa na kutafuta chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

Wizara ya Afya ya Iran leo Jumamosi imetangaza kuwa, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, wagonjwa wapya elfu mbili na 449 wa corona wamegunduliwa humu nchini. Kiujumla wagonjwa 148 wamepoteza maisha yao kwa corona katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita na wagonjwa laki moja na 98 elfu na 949 wameshapata afueni hadi hivi sasa nchini Iran na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

3471880

Kishikizo: COVID-19 iran rouhani
captcha