IQNA

Waislamu Canada watumia Ramadhani kutuma misaada ya chakula Somalia

12:34 - June 01, 2017
Habari ID: 3471003
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Canada wanachangisha pesa kusaidia familia za raia wa Somalia wanaokabilia na baa la njaa.

Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ambao Uislamu unahimiza sana kuwasiadia wasiojiweza, Waislamu kadhaa wa Canada wametenga wakati na kujitolea kuchangisha na kukusanya misaada kwa ajili ya kuwasaidia wanaokabiliwa na njaa na ukame nchini Somalia.

Taarifa zinasema Shirika la Kimataifa la Maendelea na Misaada (IDRF) lenye makao yake Canada linashirikiana na Waislamu waliojitolea kuandaa vyakula ambavyo vinapelekwa Somalia kusaidia maelfu ya familia zenye njaa.

Mkurugenzi wa idara ya kimataifa ya IDRF Farheen Khan anasema, "Ramadhani ni wakati wetu sisi kuonyesha uungaji mkono wetu kwa wenzetu na kuonyesha kuwa tunawajali wanaopata masaibu maishani." Anaongeza kuwa, kuna mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa na ni muhimu Waislamu kuonyesha kuwa wanawajali.

IDRF ambalo ni shirika la Kiislamu la kutoa misaada mara kwa mara huongoza kampeni za kimataifa za kuwasaidia watu wenye matatizo maeneo mbali mbali duniani.

Somalia ni kati ya nchi tatu za Afrika ambazo Umoja wa Mataifa umesema zinakabiliwa na mbaa la njaa. Nchi zingine ni Sudan na Nigeria. Aidha wananchi wa Yemen pia wanakabiliwa na baa la njaa.

Ukame umeyakumba maeneo mengine ya Afrika Mashariki hasa Kenya na Ethiopia ambapo watu wengi wamelazimika kuondoka makazi yao wakitafuta chakula huku watoto wengi wakikabiliwa na lishe duni.

Mpango huo wa Waislamu wa Canada wa kukusanya misaada pia unatumika kuwaelimisha watoto Waislamu nchini humo umuhimu na fadhila za kutoa sadaka.

3462995

captcha