IQNA

Watetezi wa Palestina

Afrika Kusini: Hujuma dhidi ya Rafah ni thibitisho la mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza

18:41 - February 15, 2024
Habari ID: 3478356
IQNA - Hatua za kivita za utawala wa Israel huko Rafah "zinathibitisha" usahihi wa kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala huo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema.

Alisema kile ambacho Afrika Kusini iliwasilisha kwa ICJ kilikuwa sahihi kuhusu mauaji ya kimbari.

Naledi Pandor pia alilaani kulengwa kwa wanahabari kwa ujumla na waandishi wa habari wa Al Jazeera haswa, akielezea kama kitendo cha uhalifu.

"Israel haijajizuia kufuatia uamuzi wa ICJ, na ushahidi ni kuendelea kwa vita vyake huko Rafah," waziri aliiambia Al Jazeera. "Uamuzi wa kusitisha mapigano huko Gaza uko mikononi mwa nchi zinazoipatia Israel pesa na silaha."

Kinachotia wasiwasi, aliongeza Pandor, ni kwamba Israel inaruhusiwa kupuuza uamuzi wa ICJ na kutowalinda raia.

Serikali ya Afrika Kusini imesema imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuzingatia iwapo uamuzi wa utawala wa Israel kupeleka operesheni za kijeshi Gaza hadi mji wa huko Rafah utahitaji mahakama hiyo kutumia mamlaka yake kuzuia ukiukwaji zaidi wa haki za Wapalestina.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, serikali ya Afrika Kusini ilieleza wasiwasi wake katika maombi kwamba mashambulizi ya Israel dhidi ya mji huo tayari yametokea na yatasababisha mauaji, uharibifu na maafa makubwa.

Taarifa ya Jumanne ya serikali ya Afrika Kusini imesema: "Katika ombi lililowasilishwa mahakamani 12 Februari 2024, serikali ya Afrika Kusini ilisema ina wasiwasi mkubwa kwamba mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Rafah, kama yalivyotangazwa na utawala wa  Israel, tayari yamesababisha na yatasababisha maafa makubwa zaidi, mauaji, madhara na uharibifu".

Afrika Kusini imeongeza kuwa  hatua hiyo ya utawala wa Israel  itakuwa "ni ukiukaji mkubwa na usioweza kurekebishwa wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari na Amri ya Mahakama ya ICJ tarehe 26 Januari 2024."

Mnamo Januari 26, ICJ ilitoa uamuzi kuhusu hatua za muda katika kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel kuhusu mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa iliamuru Israel kuchukua hatua za haraka kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inafika katika eneo hilo.

Afrika Kusini iliwasilisha malalamishi dhidi ya Israel katika mahakama hiyo tarehe 29 Disemba ambapo iliomba mahakama kuchukua hatua za tahadhari "kuwalinda wakazi wa Palestina dhidi ya ukiukwaji mkubwa na usioweza kurekebishwa wa haki zao chini ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari" na kuhakikisha kuwa Israel inafuata wajibu wake chini ya Mkataba huo..

Utawala dhalimu wa Israel umekuwa ukishambulia kwa makombora Rafah kwa siku kadhaa kwa maandalizi ya mashambulizi ya nchi kavu yenye lengo la kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza. Mji huo ni kimbilio la mwisho kwa Wapalestina zaidi ya milioni moja ambao waliambiwa na utawala huo huo wa Israel kuhama kusini tangu ulipoanzisha vita dhidi ya Gaza zaidi ya miezi minne iliyopita.

3487206

Habari zinazohusiana
captcha