IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani inatumia kila mbinu kuifuta Iran

22:06 - November 03, 2015
Habari ID: 3443189
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, amesema wananchi wa Iran hawatoinyooshea mkono wa urafiki Marekani ambayo inatumia kila mbinu na hila kwa lengo la kuifuta Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo mbele ya hadhara ya maelfu ya wanafunzi na wanachuo wa Kiirani kwa mnasaba wa kukaribia tarehe 13 Aban (Novemba 4) siku ya maadhimisho ya tukio lililojiri mwaka 1979 la kutekwa Pango la Ujasusi la Marekani hapa mjini Tehran. Amesema mapambano ya taifa la Iran dhidi ya Uistikbari ni mapambano ya “kimantiki, ya busara na yenye kutokana na tajiriba ya historia” na akabainisha kwamba, kinyume na maneno ya baadhi ya watu, mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wananchi wa Iran dhidi ya Uistikbari si harakati ya kijazba na isiyo na mantiki, bali inatokana na utumiaji akili, tajiriba na msukumo wa kielimu. Ayatullah Khamenei ameashiria uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran ulioanza katika miezi ya mwanzoni mwa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kwamba: baada ya Mapinduzi, Marekani iliendelea kwa muda kuwa na ubalozi Tehran, lakini haikuacha hata siku moja kufanya njama; na hii ni tajiriba ya historia, kwamba kuwa na uhusiano hakumalizi uhasama na njama za Marekani. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuelezea kushikiliwa ubalozi wa Marekani na baadhi ya wanachuo kuwa ni radiamali ya kukabiliana na njama zilizokuwa zikiendelea kufanywa na Washington na akaongezea kwa kusema: nyaraka zilizopatikana kwenye ubalozi wa Marekani zilionyesha kuwa ubalozi huo ulikuwa Pango la Ujasusi na kituo cha njama za mtawalia dhidi ya “taifa la Iran na Mapinduzi machanga ya Kiislamu”. Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba: kutokana na ufahamu wao potofu na kushindwa kuihakiki hali halisi ya Iran, kwa muda wote wa miaka 37 ya karibuni, Wamarekani wamejaribu kuuangusha Mfumo wa Mapinduzi lakini wameshindwa, na baada ya hapa pia hawatofanikiwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa laiti kama ingekuwa na uwezo, Marekani isingefanya ajizi hata kwa lahadha ndogo kuifuta Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini basira na uono wa mbali wa wananchi wa Iran ndio ulioifanya ishindwe kufikia lengo hilo.

3439932

captcha