IQNA

Ni kwa nini Saudia imekerwa na kauli ya waziri wa Lebanon kuhusu Yemen?

20:12 - November 01, 2021
Habari ID: 3474498
TEHRAN (IQNA)- Katika kulalamikia matamshi yaliyotolewa siku ya Ijumaa na George Kurdahi , Waziri wa Habari wa Lebanon aliyekosoa uvamizi wa Saudi Arabia na Imarati huko Yemen na kuutaja kuwa usio na maana, Saudia imemwita nyumbani balozi wake mjini Beirut na kumtaka balozi wa Lebanon pia aondoke nchini humo mara moja.

Kufuatia hatua hiyo ya Saudi Arabia, Bahrain nayo ambayo inaongozwa na utawala kibaraka na unaotii kikamilifu siasa na maamrisho ya Riyadh imemwita nyumbani balozi wake aliyeko Beirut. Hivi sasa Saudi Arabia ambayo inaoongoza uvamizi wa kijeshi dhidi ya nchi masiki na jirani yake Yemen tangu mwezi Machi 2015, uvamizi ambao kufikia sasa umepelekea makumi ya maelfu ya Wayemen wasio na hatia kuuawa kidhalimu na mamilioni ya wengine kupoteza makazi na kulazimika kuishi kama wakimbizi, imekwama kwenye kinamasi cha uvamizi huo isijue la kufanya. Ili kujua chanzo cha kukerwa na kila aina ya ukosoaji unaoelekezwa kwake kuhusiana na uvamizi huo, ni muhimu tuzingatie hapa nukta kadhaa:

Nukta ya kwanza ni kuwa kukerwa na hatua za pupa zisizo na busara zinazochukuliwa na Saudi Arabia kuhusu ukosolewaji unaofanywa juu ya uvamizi wake wa kijeshi huko Yemen kunatokana hasa na kukwama kwake kwenye kinamasi cha uvamizi huo. Ikumbukwe kuwa Saudia mwanzoni mwa uvamizi wake dhidi ya Yemen ilitangaza hadharani kuwa uvamizi huo haungechukua zaidi ya wiki moja kabal ya Wayemen kujisalimisha na kuwapigia magoti Wasaudi na wakati huo huo kuirudisha madarakani serikali toro ya AbduRabbuh Mansur Hadi. Kinyume na madai hayo vita vya Yemen vimeingia katika mwaka wake wa saba na wala hakuna dalili kuwa vitamalizika hivi karibuni. Hivyo Saudi imekwama kabisa kwenye kinamasi cha uvamizi wake huko Yemen na hivyo kuhatarisha itibari yake. Kwa msingi huo kukerwa huko hakutokani na nguvu bali na udhaifu mkubwa wa watawala wa Riyadh katika kukabiliana na taifa shupavu la Yemen.

Nukta ya pili ya ukerwaji huo wa kiwendawazimu inapaswa kuchunguzwa katika mtazamo wa kushindwa kwake kufikia malengo yake ya kisiasa huko Lebanon. Kwa kawaida Lebanon ni moja ya viwanja vya michezo ya kisiasa ya Saudia katika Asia Magharibi (Mashariki ya Kati). Saudia siku zote imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kuleta mabadiliko ya kisiasa Lebanon ima kupitia vibaraka wake kama vile Samir Geagea au kuchochea ghasia na machafuko moja kwa moja nchini ili kuweza kulinda maslahi yake kwa madhara ya Walebanon. Kimsingi inafanya uchochezi huo kwa ajili ya kulinda nafadi yake ya kieneo katika kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Nukta ya tatu ya kukerwa Saudia na vibaraka wake wa eneo kama vile Bahrain na matamshi ya George Kurdahi, ni kuwa akiwa Mkristo, shakhsia huyo anawakilisha Wakristo wa Lebanon na hivyo ni kipimo cha kuchukiwa Saudia na siasa zake kati ya jamii ya Wakristo wa nchi hiyo. Kwa hakika matamshi ya waziri huyo Mkristo wa Lebanon yanawashajiisha Wakristo wengine wa nchi hiyo wapate ushujaa wa kutamka na kudhihirisha wazi misimamo yao dhidi ya siasa haribifu za Saudia na vibaraka wake nchini kwao, na hilo ni jambo ambalo Saudi Arabia imekuwa ikilihofia tangu mwanzo.

Nukta ya nne ni kuwa kwa kupigia makelele na kuchukua hatua za pupa kuhusu matamshi ya George Kurdahi Saudia inafuatilia kupotosha fikra za waliowengi kuhusu masuala mengine muhimu ya kitaifa na kieneo. Moja ya masuala hayo ni ufichuaji uliofanywa na Sa'd al-Jaburi, naibu wa zamani wa mrithi wa kitu cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye alifichukua kuwa mrithi wa sasa wa kiti hicho yaani Muhammad bin Salman ni muuaji ambaye huko nyuma alipanga njama ya kutaka kumuua mfalme wa zamani wa nchi hiyo Abdallah bin Abdul Aziz.

Nukta ya tano katika uwanja huo inapaswa kutafutwa tena katika matukio ya Yemen. Hivi sasa jeshi na wapiganaji wa kamati za watu wa Yemen wamepata ushindi mkubwa katika medani za vita na hasa katika mkoa wa Marib. Kwa msingi huo Saudia imeamua kuibua makelele kuhusu matamshi ya waziri wa habari wa Lebanon ili kupotosha fikra za waliowengi ndani na nje ya eneo kuhusu hali ngumu ya kijeshi inayoikabili huko Yemen.

4009664

captcha