IQNA

Sheikh Ali Salman wa Bahrain apongeza kauli ya Mkuu wa Al-Azhar kuhusu mazungumzo ya Shia-Sunni

20:04 - November 11, 2022
Habari ID: 3476072
TEHRAN (IQNA) - Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya al-Wefaq, kundi kuu la upinzani la Bahrain, amekaribisha wito wa Shekhe Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar Sheikh Ahmed el-Tayyib wa mazungumzo ya baina ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni.

Sheikh Ali Salman, katika barua kwa Sheikh el-Tayyib, alishukuru "mwaliko wake mzuri" kwa mazungumzo mazito ya Kiislamu - Kiislamu kwa ajili ya kuunda udugu wa kidini na Kiislamu na kukataa mifarakano, migongano na mivutano  ya kimadhehebu, ofisi ya habari ya Al-Wefaq iliripoti.

Sheikh Salman pia amemshukuru Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar  cha Misri na Baraza la Wazee wa Kiislamu kwa juhudi zao za kuacha kujikita katika hitilafu na badala yake kuimarisha umoja wa Waislamu.

Amebainisha imani yake kwamba vituo vya kidini vya Kishia vitakaribisha mwaliko huu kwani daima vimekuwa vikitafuta umoja wa Kiislamu, udugu na kuishi pamoja.

Sheikh Ali Salman ameiandika barua hiyo akiwa gerezani kwani yeye ni miongoni mwa wanazuoni wa Kishia ambapo wamefungwa jela na utawala wa kiimla wa Bahrain. Wanazuoni hao wa Kiislamu na wanaharakati wengine wa kisiasa wanaoshikiliwa korokoroni ni wahanga wa ubaguzi wa kisiasa, kidini, kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kiusalama nchini Bahrain..

Akizungumza Ijumaa wiki iliyopita nchini Bahrain, Sheikh el-Tayyib alisema: “Mimi na wanazuoni wakubwa wa Al-Azhar na Baraza la Wazee wa Kiislamu tuko tayari kwa mikono miwili kuketi pamoja kwenye meza moja ya duara na ndugu zetu wa Kishia ili kuweka kando tofauti zetu na kuimarisha umoja wetu wa Kiislamu.”

Mazungumzo hayo, alisema, yatalenga kufukuza  chuki, uchochezi na kutengwa na kuweka kando migogoro ya zamani na ya sasa.

"Natoa wito kwa ndugu zangu, wanazuoni wa Kiislamu, kote ulimwenguni wa kila itikadi na madhehebu kufanya mazungumzo ya Kiislamu," al-Tayyib alisisitiza.

Alikuwa akizungumza katika kongamano lilofanyika Bahrain na kuhudhuriwa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ambaye alifanya safari yake ya kwanza kabisa katika eneo la Ghuba ya Uajemi wiki hii.

4098576

captcha