IQNA

Obama hana staritjia katika vita dhidi ya Daesh (ISIS)

13:39 - June 11, 2015
Habari ID: 3313196
Hata baada ya kupita miezi kadhaa ya kusonga mbele kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika medani za vita kwenye nchi za Kiislamu, Rais Barack Obama wa Marekani amesema kuwa serikali ya Washington bado haina stratijia kamili ya kukabiliana na kundi hilo.

Amesema serikali yake bado haijaandaa stratijia ya kuisaidia serikali ya Iraq kukomboa maeneo yaliyotekwa na kundi hilo. Huku akidai kuwa Wizara ya Ulinzi ya Marekani ingali inaandaa mbinu za kuisadia serikali ya Baghdad kutoa mafunzo na zana za kivita kwa askari wake, Rais Obama amesisitiza kwamba Wairaki wenyewe wanapasa kufanya juhudi za kupambana na Daesh. Awali katika kutoa radiamali yake kuhusiana na mafanikio makubwa ya kijeshi ya Daesh katika  mkoa wa al-Anbar nchini Iraq, Ashton Carter, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alidai kuwa askari wa nchi hiyo hawana irada na azma thabiti ya kupambana na magaidi wa Daesh.

Kuchanganyikiwa Marekani kuhusiana na mafanikio ya Daesh na makundi mengine ya kigaidi katika medani za vita huko Iraq na Syria kwa hakika kunatokana na utendaji wa nchi hiyo na vilevile siasa zake za mgongano katika Mashariki ya Kati. Mlango wa kuenea ghasia, mauaji, fujo na ugaidi nchini Iraq ulifunguliwa na Marekani yenyewe hapo mwaka 2003 ilipoamua kuivamia kijeshi nchi hiyo bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa madai yasiyo na msingi ya eti kuwepo nchini humo silaha za maangamizi ya umati. Licha ya kuwa utawala wa kibaathi wa Saddam Hussein ulikuwa utawala wa kidikteta na kiukandamizi lakini hadi sasa ahadi zilizotolewa wakati huo na Marekani za kuwaletea Wairaki demokrasia bado hazijatekelezwa hadi leo, bali kilichofanyika ni kubadilishwa kwa utawala huo wa kidekteta na uvamizi wa kijeshi. Vitendo vya kinyama vilivyotekelezwa na askari jeshi wa Marekani dhidi ya Wairaki katika maeneo kama vile Falujah na Abu Ghuraib vilizidi kuwaletea wananchi hao machungu yasiyofidika. Miaka kadhaa baadaye Marekani ilifanya njama ya kuidhibiti Iraq kijeshi, kisiasa na kiuchumi kwa kuwasilisha mipango kama vile Mashariki ya Kati Kubwa. Hatimaye askari wa Marekani walipoondoka nchini humo waliacha jeshi la taifa la Iraq likiwa limesambaratika na bila ya kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana vilivyo na changamoto pamoja na vitisho vya usalama vilivyojitokeza baadaye. Jambo hilo bila shaka liliyashawishi makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kupindukia mipaka kufanya njama za kuteka na kudhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Ni wazi kuwa matatizo ya hivi sasa ya Iraq na Syria hayatokani tu na siasa za huko nyuma za Marekani na Waitifaki wake, bali hivi sasa pia bado siasa hizo za mgongano na undumakuwili zinaendelea kutatiza na kuzua fitina katika eneo zima la Mashariki ya Kati. Kwa mfano Marekani inashambulia maeneo ya Daesh huko Syria na wakati huohuo kufanya njama za kuiangusha serikali halali ya nchi hiyo ambayo ina jeshi linaloweza kupambana vilivyo na magaidi hao. Hii ni katika hali ambayo waungaji mkono wakuu wa kijeshi na kisiasa wa Daesh ni nchi za Saudi Arabia, Qatar na Uturuki ambao ni washirika wakuu wa Marekani katika eneo. Marekani inakataa kuipa silaha za lazima serikali kuu ya Iraq huku baadhi ya wabunge wa nchi hiyo wakishinikiza kupewa silaha hizo Wakurdi na Wasuni wa nchi hiyo. Kuungwa mkono Daesh na nchi za Magharibi huko Syria kumeimarisha harakati zao za kigaidi nchini Iraq. Kwa vyovyote vile, undumakuwili wa Marekani katika kukabiliana na kundi hilo la kigaidi kumeyasababishia mataifa ya Mashariki ya Kati na hasa wananchi wa Syria na Iraq hasara na machungu mengi..../mh

3312917

Kishikizo: obama daesh iraq syria isis
captcha