IQNA

Vita dhidi ya ugaidi

Jeshi la Iran la IRGC lashambulia kwa makombora ngome za magaidi na Mossad Iraq na Syria

17:18 - January 16, 2024
Habari ID: 3478201
IQNA-Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza kuwa, limevurumisha makombora ya balestiki kulenga ngome za magaidi wa Syria, waliohusika katika mashambulizi ya hivi karibuni nchini Iran, pamoja na kituo cha ujasusi cha Israel katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Taarifa ya IRGC imesema, shambulizi la kwanza la kombora limelenga maeneo ya mikusanyiko ya makamanda na wahusika wakuu wa mashambulizi ya hivi karibuni ya kigaidi katika miji ya Kerman na Rask ya Iran.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, shambulizi hilo limetekelezwa baada ya kutambuliwa sehemu za mkusanyiko wa kundi la magaidi wakufurishaji la DAESH (ISIS) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Syria na kuteketezwa kwa makombora kadhaa ya balestiki.

Kundi la ukufurishaji la Daesh lilidai kuhusika na miripuko miwili ya mabomu iliyoua karibu watu 100 na kujeruhi wengine wengi, katika kumbukumbu ya kuuawa shahidi kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi wa Iran Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa nchi mnamo Januari 3.

Kabla ya hapo, mnamo Desemba 15, 2023 shambulio jengine la kigaidi lililenga kituo cha polisi katika mji wa Rask kusini mashariki mwa Iran, na kuua maafisa wa polisi 11 na kujeruhi wengine sita.

Katika taarifa nyingine, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limetangaza kuwa, limefanya shambulio la makombora kulenga kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad katika eneo la Kurdistan ya Iraq.

Taarifa ya IRGC imesema, shambulio hilo ni ishara ya uwezo kamili na wa hali ya juu wa kiintelijensia lililonao Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vituo na shughuli unazoendesha utawala wa Kizayuni katika eneo.

IRGC imeongeza kuwa, shambulio lake la makombora katika eneo la Kurdistan ya Iraq limekiangamiza kikamilifu kituo hicho cha Mossad katika eneo hilo.

Katika taarifa yake hiyo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limefafanua kuwa, kituo hicho cha Mossad kilitumika "kuendeleza operesheni za kijasusi na kupanga vitendo vya kigaidi" katika eneo zima, hususan nchini Iran.

IRGC imesisitiza kuwa, shambulio hilo la makombora dhidi ya kituo cha Mossad ni la kulipiza kisasi cha mauaji ya hivi karibuni ya kigaidi ya makamanda wa vikosi vya Muqawama hasa wa jeshi hilo yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni.

Taarifa hiyo imemalizia kwa IRGC kutoa hakikisho kwa "taifa adhimu la Iran" kwamba, itayanasa "makundi ya kigaidi yenye nia ovu" yanayoendesha harakati dhidi ya taifa la Iran "popote yalipo na itayaadhibu kwa vitendo vyao vya kuaibisha".

3486831

 

Habari zinazohusiana
Kishikizo: mossad iraq syria irgc
captcha