IQNA

Dunia yalaani hujuma ya ISIL dhidi ya Msikiti wa Imam Hussein AS , Saudia

15:34 - May 30, 2015
Habari ID: 3309278
Walimwengu wanaendelea kulaani hujuma ya kundi la kigaidi na Kitakfiri la ISIS au Daesh dhidi ya msikiti wa Msikiti wa Imam Hussein AS katika mji wa Dammam mashariki mwa Saudi Arabia.

Katibu Mkuu wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Kisilamu la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ISESCO Dk. Abdul Aziz Bin Othman Al-Tuwaijri amesema hujuma hiyo ya kigaidi dhidi ya msikiti inaonyesha namna magaidi hao walivyo mbali na mafundisho ya Kiislamu.

Kwingineko Shiekh Abdul Latif Daryan Mufti wa Masunni nchini Lebanon amelaani vikali hujuma dhidi ya Msikiti wa Imam Hussein AS huko Dammam Saudi Arabua na kuitaja hujuma hiyo kuwa ni hujuma dhidi ya matukufu ya Kiislamu na Waislamu. Ametoa wito kwa Waislamu kuchukua tahadhari kutotumbukia katika mtego wa fitina za kimadhehebu. Wakati huo huo Ofisi ya fatwa nchini Misri Darul-Iftaa, imelaani shambulizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh dhidi ya msikiti huo na kukitaja kitendo hicho kuwa, kinakinzana na mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Ikumbukwe kuwa jana Ijumaa watu wanne waliuawa nchini Saudi Arabia baada ya gaidi mmoja wa kundi la kitakfiri la Daesh kuulenga tena msikiti wa Mashia katika mji wa Dammam mkoa wa mashariki mwa nchi hiyo. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema hujuma hiyo imejiri katika eneo la kuegeshea magari la Msikiti wa Imam Hussein AS mjini Dammam yapata kilomita 400 kutoka mji mkuu, Riyadh. Vyombo vya habari vya Saudia vimemnukulu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani akisema gaidi aliyekuwa amejifunga mabomu, ambaye alikuwa amevaa nguo za kike, alijiripua katika eneo la kuegeshea magari msikitini hapo baada ya gari lake kusimamishwa na maafisa usalama. Gaidi aliyetekeleza hujuma hiyo aliangamia huku mpita njia pamoja na vijana wawili wa Kishia waliokuwa wakijaribu kumzuia gaidi huyo wakifa shahidi katika tukio hilo. Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza rasmi kuhusika na hujuma hiyo. Shabulio hilo la leo limekuja wiki moja tu baada ya mlipuko wa bomu ndani ya Msikiti wa Imam Ali AS katika eneo la al-Qadeeh mkoani Qatif, ambapo waumini 21 waliuawa shahidi wakiwemo watoto wawili. Matakfiri wa kundi la kigaidi la Daesh walisema wao ndio walifanya hujuma hiyo ya Ijumaa iliyopita.../mh

3309100

captcha