IQNA

Mashia na Masuni waswali pamoja Saudia kuhimiza umoja

1:46 - July 07, 2015
Habari ID: 3324232
Waislamu wa madhehebu ya Shia na wenzao wa Ahlu Sunnah, wamesali pamoja katika moja ya misikiti ya mkoa wa Qatif, mashariki mwa Saudia.

Jumapili jioni Waislamu hao walisali pamoja kwa lengo la kusisitizia umoja na mshikamano baina ya Waislamu wote. Farhan al-Shamri, Sheikh wa Ahlu Sunnah mjini Qatif ambaye alisalisha Swala ya Maghrib, amesema kuwa, kusaliwa swala hiyo kwa pamoja baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, kunaonesha mshikamano uliopo baina yao na hatua hiyo itasaidia kuzuia fitina ambazo zimekuwa zikipandikizwa na baadhi ya watu wasioutakia kheri Umma wa Kiislamu.
Kwa upande wake Sheikh Luayi al-Naser wa Kishia aliyesalisha Swala ya Isha katika swala hiyo ya umoja, amesema kuwa uelewa wa Waislamu ni jambo muhimu zaidi ili kufichua njama za maadui, na kwamba suala hilo limekuwa likilengwa na makundi ya kigaidi kuhakikisha yanavunja umoja baina ya Waislamu. Amesisitiza kuwa, swala hiyo ya pamoja, imevunja kabisa njama za vibaraka wa maadui wa Uislamu ambapo baada ya kujiri mashambulizi ya mara kadhaa ya kigaidi yaliyoua makumi ya watu, sasa Waislamu wamebaini chanzo cha fitina hiyo.
Kusaliwa swala hizo baina ya Waislamu wa Ahlu Sunnah na Shia, kuna kuja kama jibu la hatua za makundi ya kigaidi na kitakfiri ambayo yamekuwa yakijaribu kuzusha tofauti baina ya Waislamu hao. Njama za kuibua mfarakano baina ya Waislamu zimeshika kasi zaidi katika siku za hivi karibuni na zimeandamana na mauaji ya kujiripua yanayofanywa na matakfiri wa Kiwahabi.../mh

3324095

captcha