IQNA

Utawala wa Israel waendeleza hujuma dhidi ya Al Aqsa

22:49 - September 19, 2015
Habari ID: 3365118
Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleaza hujuma dhidi ya msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu.

Katika tukio la hivi karibuni Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Rami Hamdallah amezuiwa na utawala wa Kizayuni kuingia kwenye eneo la Msikiti wa al Aqsa kwa amri ya moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Jana Ijumaa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni waliuzuia ujumbe wa viongozi wa Palestina akiwemo Waziri Mkuu, Mkuu wa masuala ya usalama wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Majid Farraj na mkuu wa kitengo chake cha ulinzi, Ziyad Hab al Reeh, usiingie kwenye msikiti huo.
Kwa zaidi ya miezi miwili sasa, Israel imekuwa ikiwazuia Waislamu kuingia kwenye Msikiti huo mtukufu ambao ndicho kibla cha kwanza cha Waislamu.
Siku ya Alkhamisi, Mwanasheria Mkuu wa Israel, Yehuda Weinstein aliruhusu jeshi la utawala wa Kizayuni kutumia risasi hai dhidi ya wananchi wa Palestina wanaoandamana kupinga jinai za Israel.
Masjidul Aqsa ni eneo la tatu kwa utukufu kwa Waislamu baada ya Masjidul Haram mjini Makka na Masjidun Nabawi mjini Madina huko Saudi Arabia. Eneo linalozunguka Msikiti wa al Aqsa ni tukufu pia kwa wafuasi wa dini za Kiyahudi na Kikristo.
Kwingineko Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) imelaani vikali uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Ripoti iliyotolewa jana na ofisi ya jumuiya hiyo imesema kuwa uvamizi na siasa za utawala ghasibu wa Israel zinatishia usalama na amani ya kimataifa na imeitaja jamii ya kimataifa hususan Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake mbele ya uvamizi unaofanywa na Wazayuni huko Quds Tukufu.
Wakati huo huo balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ambaye ndiye mwenye wa sasa wa jumuiya ya NAM pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamekutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kujadili uvamizi wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa.../mh

3365097

captcha