IQNA

Jinai za Israel

OIC yasisitiza kuulinda Msikiti wa Al-Aqsa

18:27 - August 22, 2023
Habari ID: 3477482
AL-QUDS (IQNA) - Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeisitiza umuhimu wa kuhifadhi hadhi ya kihistoria na kisheria ya maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo huko al-Quds (Jerusalem).

Katika taarifa, OIC imelaani ukiukaji unaoendelea dhidi ya Msikiti unaoheshimika wa Al-Aqsa mjini al Quds na kusisitiza udharura wa jamii kimataifa kuingilia na kuuzuia utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakiuka mara kwa mara eneo hilo takatifu.

Taarifa ya OIC ilisisitiza kwamba Msikiti wa Al-Aqsa na jumba lake kubwa ni  mahali pa ibada kwa ajili ya Waislamu pekee.

Taarifa hiyo pia iliadhimisha kumbukumbu ya miaka hamsini na nne ya jaribio baya la kuuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa - alama muhimu ya kiroho kwa Waislamu, ikiwa ni Kibla cha kwanza cha Waislamu na eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu baada ya Makka na Madina.

Njama za Israel za kudhoofisha Msikiti wa  Al Aqsa

Huku kukiwa na hali ya kuongezeka kwa ukiukwaji wa sheria unaofanywa na Israel na juhudi zake za mara kwa mara za kudhoofisha hadhi ya msikiti huo, OIC imeashiria uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali, mara nyingi wakilindwa na vikosi vya Israel vinavyokalia kwa mabavu.

Vitendo hivi vimesababisha kuvunjiwa heshima kwa eneo hilo takatifu, kufungwa kwa malango yake, na mashambulizi ya kinyama dhidi ya waumini Waislamu.

Shirika hilo limesisitiza kuwa Al-Quds Al-Sharif yaani Jerusalem,  ni sehemu muhimu ya ardhi ya Palestina iliyotekwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel mwaka wa 1967. OIC imepinga kikamilifu majaribio au maamuzi yoyote yaliyolenga kubadilisha idadi ya watu au sifa za kijiografia za jiji hilo.

Dunia ikabiliane na dhulma za Israel

Katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo kuu, OIC ilitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, hasa wadau wenye ushawishi mkubwa, kushughulikia dhuluma za muda mrefu za Israel dhidi ya Wapalestina katika miongo ya hivi karibuni. Kiini cha rufaa hii ni wito wa kukomesha uvamizi wa kikoloni wa Israel na kurejesha haki halali za Wapalestina, ikiwa ni pamoja na haki yao ya kurudi katika ardhi zao za jadi zinazokaliwa kwa mabavu na walowezi wa Kizayuni..

OIC imesisitiza umuhimu wa kuanzisha taifa huru la Palestina ndani ya mipaka ya Juni 4, 1967, al Quds Mashariki ikiwa mji mkuu wake. Dira hii inawiana na maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na Mpango wa Amani wa Kiarabu - mpango wa kina ambao unashikilia ahadi ya amani endelevu.

Aidha OIC imeeleza heshima na kuvutiwa kwake na wananchi wa Palestina wenye msimamo thabiti na kusisitiza kuwa, wameendelea kuwa walinzi madhubuti na waangalifu wa ardhi na maeneo matakatifu mbele ya matatizo. Shirika hilo pia limetaka kuongezwa uungwaji mkono na mshikamano kwa al Quds na wakaazi wake wa Palestina wenye kusimama kidete.

Msimamo thabiti wa OIC unatumika kama mhimili wa kulinda utakatifu wa kidini, sheria za kimataifa, na haki za binadamu katika jiji ambalo lina umuhimu mkubwa kwa mamilioni duniani kote.

Siku ya Msikiti Duniani

Taarifa hii imetolewa kwa mnasawa wa siku ya Agosti 21, ambayo ni Siku ya Msikiti Duniani. Sababu iliyopelekea siku hii kutengwa kama Siku ya Kimataifa ya Misikiti inahusiana na tukio lililotokea miaka 56 iliyopita katika Msikiti Mtukufu wa Al-Aqsa, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel, na ambao ni Kibla cha kwanza cha Waislamu.

Saa moja asubuhi tarehe 21 Agosti 1969, Mzayuni mwenye itikadi kali kwa jina Dennis Michael William Rohan aliuchoma moto Msikiti wa Al-Aqsa kwa msingi wa hatua iliyopangwa vyema na kuungwa mkono na serikali ya wakati huo ya utawala haramu wa Israel. Kutokana na kitendo hicho cha kinyama na chuki za kidini, mitamraba 1,500 za eneo la msikiti huo ziliteketezwa.

Kufuatia kitendo hicho cha jinai, Msikiti wa Omar, Mihrabu ya Zakariya, Maqam ya Arbaeen, kumbi tatu za msikiti huo pamoja na nguzo zinazobeba kuba la Msikiti wa al-Aqsa vilichomeka kwenye moto huo, na paa la msikiti kuporomoka.

Uchomaji wa msikiti huo mtakatifu ulizua lawama na ukosoaji mkali wa kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana na kupitisha azimio nambari 271 mwaka 1969, ambalo liliulaani utawala haramu wa Israel kuhusiana na kitendo hicho.

Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia na bila kujali propaganda zilizoenezwa na utawala huo unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu na waungaji mkono wake wa Magharibi, walifanya maandamano makubwa kupinga hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni. Serikali za Kiislamu pia zilichukua hatua na kuunda "Jumuiya ya Nchi za Kiislamu" ili kukabiliana na hatari zinazotishia ulimwengu wa Kiislamu na matukufu yake.

Msikiti wa al-Aqsa unachukuliwa kuwa na utukufu wa hali ya juu katika Uislamu, na ni wa tatu kwa umuhimu baada ya Masjid al-Haram na Masjid al-Nabii. Kwa mujibu wa Riwaya, Mtume Muhammad (saw) alipanda kwenda mbinguni kutokea hapo, katika tukio la kihistoria linalojulikana kama Mi'raj, na ambalo limetajwa katika Surat al Israa katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani.

3484880

captcha