IQNA

Maandamano London, Saudia kupinga kuhukumiwa kifo Sheikh Nimr

9:22 - October 30, 2015
Habari ID: 3415411
Wanaharakati wameandamana tena nje ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini London kupinga hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama kuu dhidi ya mwanazuoni mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Nimr Baqir An-Nimr.

Wanaharakati wameandamana tena nje ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini London kupinga hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama kuu dhidi ya mwanazuoni mashuhuri wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, Sheikh Nimr Baqir An-Nimr. Waandamanaji hao siku ya Jumatano walitaka wakuu wa Saudia wabatilishe hukumu hiyo ya kidhalimu. Waandamnaji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa yameandikwa 'Free Sheikh Nimr'  yaani muachilie huru Sheikh Nimr huku wakisema anakandamizwa kwa sababu tu alipendekeza mfumo kamili wa uchaguzi Saudia.
Kwingineko wananchi wa Saudi Arabia wameandamana katika mji wa Awamiyah ulioko kwenye eneo la Qatif mashariki mwa nchi hiyo kupinga hukumu hiyo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir. Katika maandamano hayo yaliyofanyika jana, waandamanaji hao walisisitiza kuendeleza kampeni yao hiyo hadi wahakikishe hukumu hiyo inabatilishwa. Tarehe 25 mwezi huu Mahakama Kuu ya Saudi Arabia ilithibitisha hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir An-Nimr; na hukumu hiyo sasa inasubiri idhini ya saini ya Mfalme wa nchi hiyo Salman bin Abdulaziz Al Saud kwa ajili ya kutekelezwa. Endapo mfalme huyo atatoa idhini, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia inaweza kuchukua hatua ya kutekeleza hukumu hiyo ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr bila ya kutoa taarifa na indhari kabla. Siku ya Jumatatu Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu ilimwandikia barua Kamishna Mkuuwa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Zeid Al Hussein kumtaka aushinikize utawala wa Aal Saud ufute mara moja hukumu ya kifo uliyotoa dhidi ya Alimu huyo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon naye pia ameitaka Saudia isimamishe utekelezaji wa hukumu hiyo. Sheikh Nimr An-Nimr alitiwa nguvuni mwaka 2012 na kufunguliwa kesi ya kuhatarisha usalama wa utawala wa Aal Saudi kutokana na kutoa hotuba dhidi ya utawala huo na kutetea wafungwa wa kisiasa. Hata hivyo ameyakana mashtaka hayo.

3409306

captcha