IQNA

Mshikamano na Sheikh Nimr katika Sala ya Ijumaa Qatif

4:53 - December 06, 2015
Habari ID: 3460127
Waislamu katika eneo la Qatif Saudi Arabia Ijumaa hii wametoa wito wa kusitishwa hukumu ya kunyongwa mwanazuoni maarufu wa Kiislamu katika eneo hilo Sheikh Nimr Baqir An Nimr.

Katika Ijumaa iliyotajwa kuwa ya 'Mshikamano Mkubwa' Sala ya Ijumaa katika uwanja wa wazi ilisalishwa na Sheikh Abdul Karim al Jabil mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kishia Saudi Arabia.
Walioshiriki walitoa wito wa kuutaka utawala wa Aal Saudi ufute hukumu ya kifo uliyotoa dhidi ya Sheikh Nimr Baqir An-Nimr na kumwachia huru mwanazuoni huyo mwanamapambano wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia wa nchini Saudi Arabia. Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, ambaye amekuwa akipambana na utawala wa kidikteta wa Aal Saud alitiwa nguvuni mwaka 2012 na maafisa usalama wa utawala huo; na mnamo tarehe 15 Oktoba mwaka 2014 mahakama ya jinai ya Saudia ikamhukumu adhabu ya kifo mwanazuoni huyo. Tangu alimu huyo mashuhuri alipotiwa nguvuni, wananchi wa Saudia wamekuwa wakifanya maandamano makubwa ya kutaka hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya Sheikh Nimr ifutwe na mwanazuoni huyo atolewe gerezani anakoshikiliwa. Maafisa wa usalama wa utawala wa Aal Saudi wamekuwa wakitumia mkono wa chuma kuyakandamiza maandamano hayo na hadi sasa wamewakamata na kuwatia jela mamia ya waandamanaji. Wananchi Waislamu wa Kishia nchini Saudia wanalalamika kuwa hukumu iliyotolewa na utawala wa Aal Saudi dhidi ya Sheikh Nimr pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa si za kiadilifu bali hukumu hizo zinalenga kuwaadhibu na kuwakomoa Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Katika ujumbe wao waliotoa, wanaharakati na wanamapinduzi wa Saudia, wametangaza mshikamano wao na Sheikh Nimr Baqir An-Nimr na kusisitiza kwamba kwa kumnyonga mwanazuoni huyo, utawala wa Aal Saudi hautoweza kuwakomoa wanaharakati wa kisiasa na kuzima upinzani na malalamiko yao wanayoyabainisha kwa njia za amani. Katika ujumbe wao huo, wanaharakati hao wamesema, kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni huyo mwanamapambano, kutazidisha tu wimbi la harakati halali na za kisheria za wananchi wa Saudia za kupigania haki zao dhidi ya utawala muuaji wa ukoo wa Aal Saud. Hayo yanajiri katika hali ambayo, maulama wa Kiislamu nchini Lebanon wametoa taarifa, ambapo mbali na kutahadharisha juu ya matokeo hasi yatakayotokana na kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi ya Sheikh Nimr Baqir An-Nimr, wameutaka utawala wa Saudia umwachie huru alimu huyo. Taarifa ya maulama wa Lebanon imesisitiza kwamba Sheikh Nimr hajafanya kosa lolote la uhalifu bali ametiwa gerezani kwa sababu ya kubainisha imani na itikadi yake. Maulama hao wamezitaka jumuiya na asasi za kieneo na kimataifa za kutetea haki za binadamu ziishinikize Saudia imwachilie huru Sheikh Nimr. Ayatullah Ali Sistani, Marjaa Taqlidi wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq naye pia ametuma ujumbe kwa utawala wa Riyadh wa kuutaka ufute hukumu ya adhabu ya kifo uliyotoa dhidi ya Sheikh Nimr. Ripoti zinaeleza kuwa tangu Sheikh Nimr alipokamatwa na kutiwa jela, utawala wa Aal Saud umejaribu bila mafanikio kudhoofisha moyo wa mwanazuoni huyo; na licha ya kutolewa ripoti za kila leo kuhusu kukaribia siku ya kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi yake, Sheikh Nimr angali na moyo thabiti na amejiweka tayari kukabiliana na hali yoyote ile. Sambamba na hayo, ripoti kutoka nchini Saudia zinaeleza kuwa utawala wa Aal Saud umeendeleza jinai na ukandamizaji wake dhidi ya Waislamu wa Kishia, baada ya kuwahukumu vijana wanne wa Kishia kifungo cha kati ya miaka 13 hadi 25 jela mbali na marufuku ya kusafiri nje ya nchi kwa tuhuma za kushiriki kwenye maandamano mbalimbali ya kupinga utawala huo…/

3459719

captcha