IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qu’rani ya Wanachuo Waislamu, Tukio la Kipekee

11:58 - July 10, 2016
Habari ID: 3470445
Katibu wa Baraza la Ustawi wa Utamaduni wa Qur’ani Iran amesema Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu ni tukio la kipekee katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Hujjatul Islam Hamid Muhammadi amesema, mashindano hayo ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu duniani yana hadhi ya juu hata zaidi ya mashindnao ya kimataifa ya Qur’ani nchini Iran.

Amesema wanaoshiriki katika mashindano ya kimatiafa ya Qur’ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aghalabu huwa wamebobea tu katika masuala ya Qur’ani lakini wale wanoshiriki katika Mashindano ya Kimatiafa ya Qur’ani ya wanachuo, mbali na kuwa wataalamu wa kuhifadhi na kusoma Qur’ani pia huwa wataalamu katika taaluma mbali mbali za sayansi na elimu.

Aidha amepongeza jitihada za Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR) ambayo huandaa mashindano hayo ya Qur’ani ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu.

Amesema kwa kuzingatia harakati makundi yenye misimamo mikali ya kitakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu, mashindano kama hayo ya wanachuo ni njia mojawapo za kukabiliana na harakati za makundi hayo potovu.

Hujjatul Islam Muhammadi amesema Baraza la Ustawi wa Utamaduni wa Qur’ani Iran amesema litafanya kila liwezalo kufanikisha Duru ya 6 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu.

Amesema kwa kuzingatia kuwa mji mtakatifu wa Mashhad utakuwa mwenyeji wa mashindano hayo, inatazamiwa kuwa mashindano hayo yatafana sana kwa kuzingatia hadhi ya mji huo. Mashindano hayo yanatazamiwa kufanyika Januari 1-4 mwaka 2017 katika mji huo ulio kaskazini mashariki mwa Iran.

Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR) imekuwa ikiandaa mashindano ya Qur’ani ya wanachuo Waislamu baada ya kila miaka miwili tokea mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano baina ya wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu kote duniani sambamba na kustawisha kiwango cha harakati za Qur’ani katika vyuo vikuu.

3503363

captcha