IQNA

Mapambano ya Wapalestina

Ismail Haniya: Muqawama wa Wapalestina umebaki imara

18:33 - December 20, 2023
Habari ID: 3478066
IQNA - Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya Palestina, Hamas, Ismail Haniya amesisitiza uthabiti na azma la harakati hiyo katika kuendeleza mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina.

Akizungumza katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian mjini Doha, Qatar, Haniya alieleza mashambulizi ya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza kutoka nchi kavu, angani na baharini kuwa hayajawahi kushuhudiwa lakini akasisitiza kuwa wameshindwa kuiangusha harakati ya Hamas.

Baada ya siku 75 za ukatili na jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza, muqawama umeendelea kuwa imara na wenye nguvu na umesababisha hasara kubwa kwa adui, alisema.

Amesema maelfu ya watu wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa shahidi au kujeruhiwa na maelfu ya nyumba na majengo yameharibiwa katika mashambulizi ya Israel lakini wananchi wa Palestina wanaendelea na njia ya muqawama ili kuushinda utawala wa Kizayuni.

Katika kikao chao, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kiongozi hiyo Hamas walibadilishana mawazo kuhusu matukio ya hivi punde ya Palestina, hususan katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Wakati huo huo, shirika la habari la Urusi RT Arabic liliripoti kwamba Haniya atasafiri kwenda Misri kwa mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza.

Bado hakuna maelezo yoyote yaliyofichuliwa kuhusu safari hiyo lakini harakati ya muqawama wa Palestina tayari imefutilia mbali mabadilishano ya wafungwa na utawala wa Kizayuni maadamu vita vinaendelea.

Vyombo vya habari vya Israel vimedai kuwa kuna mazungumzo mazito yanaendelea kuhusu kubadilishana wafungwa lakini mpango huo haujakaribia.

Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kikatili katika Ukanda wa Ghaza tokea tarehe 7 Oktoba, vita ambavyo kwa mujibu wa maafisa wa Palestina na duru za Umoja wa Mataifa, mbali na kusababisha maafa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa, vimeharibu miundombinu mingi na kuua shahidi maelfu ya raia, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake.

Utawala huo ghasibu bado unaendeleza hujuma zake hizo katika maeneo yote ya Ukanda wa Ghaza ambapo takwimu za karibuni kabisa zinaonesha kuwa zaidi ya Wapalestina 19,400 wameshauawa shahidi na zaidi ya 52,200 wengine wameshajeruhiwa hadi hivi sasa.

Habari zinazohusiana
captcha