IQNA

Malamiko India baada mwanafunzi Muislamu kuhujumiwa na wahuni kwa kuvaa hijabu

22:20 - February 09, 2022
Habari ID: 3474910
TEHRAN (IQNA)- Klipu iliyowekwa kwenye mtandao wa Twitter ikimuonyesha mwanafunzi Muislamu aliyevaa hijabu akibughudhiwa kwa maneno na genge la wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka katika chuo kimoja cha jimbo la Karnataka nchini India, imezusha moto wa hasira na kuzidisha malalamiko ya kupinga marufuku ya uvaaji hijabu iliyowekwa katika taasisi za elimu za jimbo hilo.

Malamiko India baada mwanafunzi Muislamu kuhujumiwa na wahuni kwa kuvaa hijabuKatika video hiyo anaonekana binti Muislamu Muskan Khan akiwa amezungukwa na wanaume waliovaa mitandio ya Kihindu ya rangi ya zafarani walioanza kumshambulia kwa maneno alipowasili katika chuo cha eneo la Mandya katika jimbo hilo.

Muskan Khan ameieleza chaneli ya televisheni ya NDTV ya India kuwa, alikuwa amekwenda chuoni hapo kukabidhi kazi yake ya masomo, wakati wanaume hao, ambao wengi wao amesema, si wanafunzi wa chuo hicho, walipomzuia asiingie chuoni kwa sababu amevaa hijabu.

Amesema, baada ya hapo walianza kupiga nara za kumtukuza 'mungu' wao wa Kihindu, na yeye akaanza kupiga takbir huku akisisitiza kuwa ataendelea kupigania haki yake ya kuvaa vazi hilo la staha la Kiislamu.

Marufuku ya kuvaa hijabu iliyowekwa katika vyuo vya jimbo la Karnataka imeamsha wimbi la hasira za wanafunzi Waislamu, ambao wanasema, hiyo ni hujuma inayolenga imani yao ambayo inatambuliwa rasmi na katiba ya India, huku makundi ya Kihindu ya mrengo wa kulia yakitumia mabavu kuwazuia mabanati wa Kiisalmu wasiingie vyuoni na hivyo kuibua mivutano ya kijamii jimboni humo.

Serikali ya jimbo la Karnataka inayoongozwa na chama cha mrengo wa kulia cha Bharatiya Janata (BJP) jana ilitangaza kufunza taasisi za elimu kwa muda wa siku tatu.

Mwezi uliopita, wanafunzi katika chuo kimoja cha serikali waliamriwa kutovaa hijabu katika jimbo hilo ambalo asilimia 12 ya wakaazi wake ni Waislamu.

Vyombo vya habari vya jimbo la Karnataka  vimeripoti kuwa skuli kadhaa katika mji wa pwani wa Udupi nazo pia zimewazuia wasichana Waislamu wanaovaa hijabu wasiingie ndani ya skuli kwa kisingizio cha kutekeleza amri ya wizara ya elimu ya jimbo hilo, kitendo ambacho kimezusha malalamiko ya wanafunzi na wazazi wao.

4034740

Kishikizo: india waislamu hijabu
captcha