IQNA

Sikukuu ya Idul Fitr

Kiongozi Muadhamu katika Sala ya Idul Fitr: Irada ilioimarika kitaifa itatatua matatizo

11:53 - April 22, 2023
Habari ID: 3476901
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba za Sala ya Idul Fitr amesisitiza kuwa, irada iliyoimarika kitaifa itatatua matatizo ya nchi.

Sala ya Idul Fitr leo mjini Tehran imesalishwa na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Eneo la Sala la Imam Khomeini (MA).

Katika hotuba yake ya kwanza ya Sala, Ayatullah Khamenei ametuma salamu zake za pongezi za sikukuu ya Idul Fitr kwa umma wa Kiislamu duniani na taifa la Iran na huku akichambua harakati adhimu ya taifa katika Siku ya Kimataifa ya Quds Ijumaa wiki iliyopita baada ya kubakia macho usiku kuhuisha Usiku wa Qadr amesema: "Mjumuiko huo mkubwa na mtukufu kwa hakika ulikuwa ni katika neema na taufiki ya Mwenyezi Mungu".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, mshikamano, kuhurumiana na kusaidiana mihimili mitatu ya dola ni mkakati muhimu sana na wa msingi katika kutatua matatizo na kustawisha nchi. Huku akiashiria utaratibu mzuri wa katiba kuhusu kuundwa mihimili mitatu ya dola nchini Iran amesema: "Iwapo mihimili hiyo ambayo ni Bunge, Serikali, na Idara ya Mahakama itashirikiana kikamilifu, hakutakuwa na mkwamo popote pale na wakuu na wakurugenzi katika mihimili hiyo wanafahamu ni vipi waibue ushirikiano huo."

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, mkakati wa adui ni kuibua mifarakano na migongano na kuongeza kuwa: "Adui anajaribu kuhakikisha wananchi wanapigana na wanazozana kutokana na  kuwa na itikadi na misimamo inayotofautiana. Lakini ifahamike kuwa, kuwepo mitazamo tofauti baina ya wananchi katika masuala mbali mbali ni jambo lisilo na pingamizi na hilo halipaswi kuwa chanzo cha mizozo na migogoro. Badala yake, kwa kubatilisha vishawishi vya adui vya kuwafanya wananchi wasiwe na mtazamo mzuri baina yao kwa wao huku wakiwa  na mtazamo mbaya kwa maafisa wa nchi, tunapaswa kuishi pamoja na kuwa wema."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kusambaratika stratijia ya kijeshi ya adui katika eneo na kusema: "Adui  huyo sasa amegeukia sera ya udanganyifu, upotoshaji, uwongo, vishawishi, udhalilishaji na kuyafanya mataifa yawe na mtazamo mbaya kuhusu  uwezo wao."

Ayatullah Khamenei amesema inapaswa kusamabratisha mikakati ya adui kwa kufahamu kikamilifu mbinu anazotumia.

Amesisitiza kuwa: "Taifa lenye busara na nguvu la Iran ambalo hadi leo limezishinda njama zote za maadui , litaendelea kuwakatisha tamaa maadui hao kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu."

4135866/

captcha