IQNA

Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran

Operesheni ya IRGC ni onyo kwa utawala wa Kizayuni kuhusu uwezo wa makombora ya Iran

22:17 - January 19, 2024
Habari ID: 3478219
IQNA-Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya leo hapa mjini Tehran amesema shambulio la makombora la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) dhidi ya kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel (Mossad) katika eneo la Kurdistan ya Iraq limetoa onyo kali mkabala wa tishio la Wazayuni.

Hujjatul Islam Kazem Sediqi ameashiria mashambulio hayo ya IRGC ya makombora ya balestiki dhidi ya ngome za magaidi wa Syria, waliohusika katika mashambulizi ya hivi karibuni nchini Iran, pamoja na kituo cha ujasusi cha Israel katika eneo la Kurdistan ya Iraq na kusema: Hujuma hizo zimetoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni, ili ufahamu kuwa makombora Iran yanaweza kuupiga utawala huo.

Ameeleza bayana kuwa, shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha ujasusi cha shirika la ujasusi la utawala wa Kizayuni wa Israel Mossad katika eneo la Kurdistan limempa onyo adui Mzayuni, huku likimtaka akomeshe vitendo vyake vya kigaidi katika eneo.

Hujjatul Islam Sediqi amebainisha kuwa, mashambulio hayo ya IRGC yalifanywa kwa niaba ya wananchi shupavu wa Iran ili kuwaonya wasioitakia mema Iran ya Kiislamu na kuwafahamisha kuwa, wakifanya jinai mkabala wa taifa hili, wataadhibiwa.

"Hawana sehemu yoyote salama wala popote pa kukimbilia duniani," ameongeza Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo hapa mjini Tehran.

Kadhalika Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amekumbusha kuwa, kadhia ya Gaza ndilo suala muhimu zaidi hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu, na kwamba wenye fikra huru duniani wataendelea kuwa pamoja na wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Amesema zaidi ya siku 100 zimepita tangu Wazayuni waanzishe mashambulio ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, utawala huo katili unaendelea kukanyaga sheria zote za kimataifa mkabala wa kimya cha jamii ya kimataifa. 

Kwengineko katika hotuba zake za Ijumaa hii leo, Hujjatul Islam Sediqi  amesema hakuna shaka kwamba wananchi wa Iran, kama walivyofanya katika chaguzi zote zilizopita baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979, watashiriki pia kwa wingi katika uchaguzi wa awamu ya kumi na mbili ya Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran (Bunge) na awamu ya sita ya Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi utakaofanyika tarehe Pili Machi mwaka huu.

captcha