IQNA

Waislamu India

Wahindu waendeleza chuki dhidi ya Waislamu India kwa himaya ya utawala

16:27 - April 27, 2023
Habari ID: 3476921
TEHRAN (IQNA)- Serikali ya India yenye misimamo ya kufurutu ada imefuta historia ya watawala wa Kiislamu katika vitabu vya masomo na kuzidi kuthibitisha kwamba, inafuatilia kwa nguvu zote siasa za kukabiliana na Waislamu pamoja na historia yao.

Baada ya Waziri Mkuu Narendra Modi mwenye mielekeo ya kihindu kushika hatamu za uongozi nchini India siasa za chuki dhidi ya Uislamu za serikali ya New Delhi zilishika kasi na kuchukua wigo mpana zaidi. Mwenendo huo umeongezeka mno kiasi kwamba, Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa wakivamia na kushambulia misikiti na nembo za Kiislamu bila ya woga wowote ule. Katika mlongongo huo, hivi karibuni Wahindu wenye misimamo mikali walichoma moto maktaba ya kihistoria ya Waislamu katika jimbo la Bihar ambayo ina ukongwe wa miaka 113.

Hii ina maana kwamba, pamoja na hatua za kimaonyesho za Waziri Mkuu Narendra Modi za kushirikiana na Waislmau, lakini Wahindu ambao wanaungwa mkono na serikali yake ya chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) wanaendelea kutenda jinai zao dhidi ya Waislamu. Rajiya Singh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili kwamba:

Vyama vyenye misimamo mikali na ya kufurutu ada vya India kama RSS na Shiv Sena vina himaya na uungaji mkono kamili wa serikali ya India na ndio maana vimekuwa vikifanya kila jinai dhidi ya Waislamu na kutokuwa na wasiwasi wowote. Viongozi wa Kiislamu nchini India wametahadharishha mara chungu nzima katika mazungumzo yao na viongozi wa serikali ya New Delhi kuhusiana na matokeo mabaya ya vitendo vya Wahindu vya kuvunjia heshima nembo za Kiislamu sambamba na hujuma dhidi ya wafuasi wa dini hii.

Pamoja na hayo, kufutwa historia ya Waislamu katika vitabu vya masomo vya India ni hatua inayoonyesha ni kwa kiasi gani chuki dhidi ya Uislamu zinavyofanywa na serikali ya India zimechukua wigo mpana tena kwa sura rasmi. Baraza la Taifa la Uhakiki wa Malezi na Masomo la India lenye jukumu la kuandaa mitaala na rariba za masomo ya shule na vituo vya elimu, limechukua hatua ya kufuta faslu na milango inayohusiana na historia ya watawala wa Kiislamu katika karne ya 19 nchini humo na kuiondoa kabisa katika vitabu vya masomo.

4133425

Kishikizo: india waislamu modi
captcha