IQNA

Watetezi wa Palestina

Afrika Kusini yaifikisha Israel katika mahakama ya ICJ kuhusu mauaji ya kimbari Gaza

9:58 - December 30, 2023
Habari ID: 3478112
IQNA-Afrika Kusini imefungua kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kuhusu mashambulizi ya "mauaji ya kimbari" ya utawala huo dhidi ya Gaza, ambayo hadi sasa yameua zaidi ya Wapalestina zaidi ya 21,500.

Taarifa ya kesi hiyo inasema hatua za Israel ni "mauaji ya kimbari kwa sababu zina nia ya kuleta uharibifu wa sehemu kubwa ya kundi la taifa, rangi na kaumu ya Palestina."

Aidha Afrika Kusini imesema: "Vitendo vinavyozungumziwa ni pamoja na kuwaua Wapalestina huko Gaza, na kuwasababishia madhara makubwa ya kimwili na kiakili, na kuwasababishia hali ya maisha iliyokadiriwa kuwaangamiza kimwili."

Ombi hilo lilisema mashambulizi ya Israel yanakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mauaji ya Kimbari, na mahakama imetakiwa "iamuru Israel isitishe mauaji na kusababisha madhara makubwa ya kiakili na kimwili kwa Wapalestina huko Gaza."

Aidha ombe la Afrika Kusini kwa ICJ limebaini kuwa  "Israel imejihusisha, inajihusisha na inatishia  kushiriki zaidi katika vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina huko Gaza."

Ombi hilo liliitaka mahakama "kuiamuru Israel kusitisha mauaji na kusababisha madhara makubwa ya kiakili na kimwili kwa watu wa Palestina huko Gaza."

Wizara ya mambo ya nje ya utawala haramu wa Israel ilisema inapinga kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini katika mahakama ya ICJ.

Serikali na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamelaani mauaji ya kimbari ya yanayotekelezwa na Israel kwa himaya ya Marekani huko Gaza na kutaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike kuhusiana na mauaji hayo.

Afrika Kusini imekuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Wapalestina na imechukua hatua kadhaa kuiwajibisha Israel kwa vitendo vyake huko Gaza.

Wabunge wa nchi hiyo mwezi uliopita walipiga kura ya kuunga mkono kufungwa kwa ubalozi wa utawala Israel mjini Pretoria na kusimamisha uhusiano wote wa kidiplomasia hadi uvamizi dhidi ya Gaza utakapokoma.

Mwezi Novemba, Afrika Kusini iliipeleka Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ambayo tayari imesema imeanzisha uchunguzi kuhusu jinai za Israel dhidi ya Wapalestina.

Afrika Kusini imeunga mkono hoja ya Wapalestina ya kuwa taifa katika maeneo yanayokaliwa na Israel kwa miongo kadhaa, ikifananisha masaibu ya Wapalestina na yale ya Waafrika wazalendo walio wengi nchini Afrika Kusini wakati wa enzi ya ukandamizaji wa utawala wa ubaguzi wa rangi au apathaidi.

ICJ ni mojawapo ya vyombo sita vikuu vya Umoja wa Mataifa na husaidia kutatua migogoro kati ya mataifa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

3486608

Habari zinazohusiana
captcha