IQNA

Matukio ya Palestina

UN: Israel imeua watoto wengi zaidi Ukanda wa Gaza miezi mitano iliyopita

11:40 - March 14, 2024
Habari ID: 3478514
IQNA-Francesca Alnanese Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina alisema jana katika ripoti kali iliyowasilishwa kwa umoja huo kuwa Israel imeua watoto wengi zaidi katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Amesema idadi hiyo ya vifo ni kubwa kuwahi kushuhudiwa katika mizozo yote duniani iliyojiri katika kipindi cha miaka minne ya karibuni. Francesca Albanese amekosoa hali ya mgogoro inayousibu Ukanda wa Gaza na kusema kuwa kile kinachojiri katika eneo hilo ni mchakato wa kimfumo ambao ni sawa na mauaji ya kimbari. 

Ripoti ya Albanese inasisitiza kuhusu hali halisi ya kutisha inayowakabili watoto wa Kipalestina chini ya uvamizi wa Israel, ikionyesha hali mbaya ya mzozo huo. Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ameandika katika ukurasa wake wa X kwamba: "Kuangamiza idadi ya watu kutoka kwenye asili yake. Mauaji ya kimbari ni mchakato, na kinachotokea Gaza ni janga lililotabiriwa."

Ripoti hiyo kali ya Francesca Albanese kwa Umoja wa Mataifa imeweka wazi mashambulizi yasiyosita ya Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza khususan watoto ambao ni wahanga wakuu wa jinai hizo. 

Zaidi ya Wapalestina 31,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wameuawa shahidi huko Gaza, na wengine zaidi ya 73,000 kujeruhiwa tangu utawala haramu wa Kizayuni uanzishe mashambulizi ya kikatili dhidi ya eneo hilo Oktoba 7 mwaka jana huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu, ukosefu wa chakula na mahitaji mengine muhimu. 

HAMAS yakanusha madai ya kuafiki pendekezo la usitishaji vita

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekadhibisha ripoti ya shirika la habari la al-Arabiya kwamba kundi hilo la muqawama limeafiki 'pendekezo la kimataifa' la usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa, HAMAS imepuuzilia mbali ripoti hiyo ya al-Arabiya ikisisitiza kuwa, chombo hicho cha habari kinapasa kuhakikisha kuwa habari kinazochapisha ni za uhakika, ukweli na za kuaminika.

Harakati hiyo ya muqawama ya Palestina imebainisha kuwa, vyombo vya habari vina wajibu wa kujiepusha na tabia ya kucheza na hisia za watu hasa Wapalestina, wakati huu ambao jeshi la utawala wa Kizayuni linaendelea kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

HAMAS imesisitiza kuwa, ripoti ya shirika la habari la al-Arabiya kwamba ujumbe wa HAMAS ndani ya siku chache zijazo utaelekea Cairo, Misri kujadili na kusaini makubaliano ya kuanza kutekeleza kile kilichotajwa kuwa pendekezo la kimataifa la usitishaji vita, haina itibari

Kabla ya hapo, Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS alisema hakutakuwa na makubaliano yoyote na utawala haramu wa Israel kabla ya utawala huo pandikizi kusimamisha kikamilifu hujuma zake dhidi ya Ukanda wa Gaza na kuyaondoa majeshi yake katika eneo hilo.

"Hatutaki makubaliano ambayo hayatamaliza vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza au kuhakikisha watu wetu waliofukuzwa makwao wanarejea katika makazi yao, au makubaliano ambayo hayatoi hakikisho la kuondoka kwa adui Mzayuni katika Ukanda wa Gaza", alisema Ismail Haniyah.

Hali mbaya katika magereza ya kuogofya ya Israel

Katika taarifa yake, Klabu ya Mateka wa Palestina imetahadharisha kuhusu hali mbaya ya mateka hao wanaoshikiliwa katika jela za utawala wa kibaguzi wa Israel.

Kabla ya kuanza vita vya Ghaza tarehe 7 Oktoba 2023, idadi ya mateka wa Kipalestina katika jela za Kizayuni ilikuwa karibu 5,000. Idadi ya mateka hao imeongezeka mara mbili katika kipindi cha miezi 5 iliyopita, ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza. Kwa mujibu wa tangazo la klabu hiyo ya mateka wa Palestina, Wapalestina 9100 (wakiwemo watoto na wanawake) wanashikiliwa katika jela za kutisha na zenye hali mbaya sana za utawala wa huo ghasibu wa Kizayuni.

Mbali na mauaji ya kimbari huko Gaza, utawala  wa Israel pia umezidisha ukatili wake dhidi ya wafungwa wa Kipalestina. Suala hili pia limeashiriwa katika taarifa ya klabu hiyo ya mateka na wafungwa wa Palestina. Inaeleza kuwa tangu kuanza kwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, idara ya magereza ya Israel imezidisha mateso dhidi ya wafungwa wa Kipalestina.

 Maandamano Jordan

Maandamano ya kuinga mkono Palestina yamefanyika karibu na ubalozi wa utawala wa Kizayuni huko Amman mji mkuu wa Jordan.

Mamia ya wananchi wa Jordan wakazi wa mji mkuu wa nchi hiyo wameandamana karibu na ubalozi wa utawala wa Israel huko Amman kuiunga mkono Palestina. Waandamanaji walikuwa wakipiga nara" tunajitolea nafsi na roho zetu kwa ajili ya Palestina, na " Ukanda wa Gaza hauko peke yake; "Wajordani wote wako pamoja na Hamas."  

Yanal Freihat, mjumbe wa bunge la Jordan, amewaambia waandishi wa habari: Washiriki katika maandamano ya jana wawametaga utiifu wao kwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina  (Hamas) na brigedi zote za muqawama huko Ukanda wa Gaza, na kwamba wananchi wote wa Jordan  wako pamoja na muqawama wa Palestina.  

 Wazayuni watoroka vita

Makumi ya maelfu ya walowezi wa Kizayuni wamekimbia makazi yao katika maeneo ya kaskazini mwa Palestina yaliyopachikwa jinai bandia la Israel, wakihofia mashambulizi ya Harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

Jenerali Tamir Hayman, mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya jeshi la utawala haramu wa Israel amesema walowezi 80,000 wa Kiyahudi wamelazika kuyakimbia makazi yao katika maeneo ya kaskazini, baada ya kutiwa wahaka na hujuma za makombora ya Hizbullah.

Jenerali Hayman amekiri kuwa, kuendelea kwa mashambulizi ya Hizbullah katika maeneo hayo ya kistratajia yaliyoko mpakani na Lebanon ni kwa maslahi ya mrengo wa mapambano ya Kiislamu. 

Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon kwa miezi kadhaa sasa umeendelea kupiga kwa makombora kambi za kijeshi na maeneo mengine ya Kizayuni huko kaskazini mwa Palestina yaliyopachikwa jinai bandia la Israel.

 

4205377

Habari zinazohusiana
captcha